Rio Ferdinand hatacheza dhidi ya Benfica

Rio Ferdinand hakusafiri na kikosi cha Manchester United kilichoelekea Ureno kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya hekaheka za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Benfica siku ya Jumatano.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Rio Ferdinand

Mlinzi huyo wa kati hajaumia upya na badala yake amepumzishwa kwenda Ureno na alicheza dakika tisini kwa mara ya kwanza msimu huu siku ya Jumapili.

Beki waliyezoeana katika nafasi hiyo ya ulinzi wa kati Nemanja Vidic pia hatacheza mchezo huo, kwa hiyo Jonny Evans itambidi kwa mara nyingine ashirikiane na Phil Jones kuimarisha safu ya ulinzi.

Michael Owen amejumuishwa katika kikosi kilichokwenda Ureno, lakini Mame Biram Diouf na Federico Macheda hawamo.

Ingawa Ferdinand na Vidic bado wataendelea kuwa chaguo la kwanza katika safu ya ulinzi wa kati kwa Manchester United, timu hiyo haijakumbwa na matatizo ilipowakosa wachezaji hao, wakati Ferdinand alipokuwa na matatizo ya mgongo huku Vidic akiwa ameumia misuli gotini.

Wakati walipokuwa wakijiuguza, Evans na Jones wamekuwa moyo wa ulinzi ambapo Man United walifungwa mabao matatu tu katika mechi nne, wakati klabu hiyo ikiwa imeshinda mechi zake zote nne walizocheza za Ligi Kuu ya England wanashikilia usukani.

Wakati Chelsea ndio timu itakayoelekea uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili, Sir Alex Ferguson atahitaji kutumia vizuri wachezaji alionao ingawa inaaminika atawatumia wachezaji wenye uzoefu zaidi dhidi ya timu iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi ya Ureno msimu uliopita.