Van der Vaart achukia kuondolewa Europa

Kiungo mshambuliaji wa Tottenham Rafael van der Vaart amesema amekasirika kuachwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki Ligi ya Europa.

Image caption Rafael van der Vaart

Van der Vaart alitoka akichechea wakati Spurs iliposhindiliwa mabao 5-1 na Manchester City na awali ilielezwa asingeweza kucheza kwa muda wa wiki sita akiuguza msuli wa paja.

Lakini licha ya sasa akiwa anatarajiwa kupona na kuweza kucheza mechi dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili, kuenguliwa kwake kuna maana mchezaji huyo atakosa mechi sita za makundi za ligi ya Europa.

"Spurs wangeweza kushauriana nami," alieleza katika mtandao wake rasmi binafsi.

Amesema zaidi: "Nadhani ni suala la aina yake."

Hata hivyo amesema hayo anayapa kisogo na anajiandaa kwa pambano dhidi ya Liverpool na ameonesha matumaini atakuwa amepona kabisa hadi wakati huo.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alikosa kuiwakilisha nchi yake ya Uholanzi kwa mashindano ya kufuzu kwa Euro 2012 na pia hakupangwa katika mechi ya kwanza kwa Spurs kushinda msimu huu dhidi ya Wolves siku ya Jumamosi.

Meneja wa Spurs Harry Redknapp anakusudia kuchezesha damu changa kama Harry Kane, Tom Carroll na Jake Livermore katika Ligi ya Europa ili kukiweka kikosi chake tayari kwa ajili ya patashika za Ligi Kuu ya England.

Spurs wataanza mtanange wa Ligi ya Europa League dhidi ya PAOK Salonika nchini Ugiriki siku ya Alhamisi.

Iwapo watafanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi, wataruhusiwa kusajili wachezaji wengine watatu wapya.