Niger yasambaratisha msafara wa al-Qaeda

Ramani ya Niger
Image caption Ramani ya Niger

Jeshi la Niger, lililokuwa likishika doria, limeshambulia msafara uliokisiwa kuwa na wapiganaji wa al-Qaeda na kuwaua watu watatu, kwa mujibu wa Waziri kutoka Wizara ya Ulinzi.

Mahamadou Karidio alisema shambulio hilo lilfanyika eneo la Agadez, kwenye jangwa kaskazini mwa nchi hiyo.

Silaha zilipatikana na watu zaidi ya 50 waliokuwa wamesajiliwa kwa lazima walikamatwa, alisema.

Kundi la al-Qaeda Islamic Maghreb (AQIM) limekuwa likiendesha shughuli zake nchini Niger, Mali na Algeria wakiwateka nyara watu kwa ajili ya kudai kikombozi.

Inasadikiwa kuwa kundi hilo limekuwa likiwasajili wanavijiji kwa kuwapa magari na pesa, kulingana na taarifa za shirika la habari la Associated Press.

Lakini taarifa ya waziri inaashiria kuwa baadhi ya wapiganaji walilazimishwa kujiunga na kundi hilo.

Bw Karidio aliiambia AP kuwa 'vijana waliookolewa' wanapelekwa mji mkuu Niamey ili kuhojiwa.

AQIM liliibuka, wakati wa vita vya miaka ya 90 nchini Algeria, kama kundi la madhehebu ya Salafi inayohubiri dini na kupambana.

AQIM lilitangaza kuiunga mkono al-Qaeda miaka mitano iliyopita na kubadilisha jina lake.