Al Ahly yatolewa ubingwa wa Afrika

Mabingwa mara sita wa soka barani Afrika Al Ahly wametolewa katika mbio za Ligi ya Ubingwa wa Afrika baada ya kwenda sare ya 1-1 na Esperance ya Tunisia katika mchezo wa mwisho wa kundi B.

Image caption Wachezaji wa Al Ahly

Kwa matokeo hayo Ahly wanaweza kufikisha pointi saba na watamaliza katika nafasi ya tatu, wakati Esperance wamemaliza kileleni kwa kufikisha pointi 10.

Kutolewa kwa Ahly pia kulizidi kushindiliwa baada ya klabu ya Morocco ya Wydad Casablanca ilipofungwa mabao 3-1 na Mouloudia Alger ya Algeria katika mechi nyingine ya kundi hilo.

Wydad imemaliza ikiwa imevuna pointi saba mbele ya mabingwa hao wa Misri kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Matokeo ya mwisho yatajulikana siku ya Jumapili wakati Enyimba ya Nigeria itaikaribisha Cotonsport ya Cameroon na Al Hilal ya Sudan itakapokuwa wageni wa Raja Casablanca ya Morocco.

Enyimba tayari imekwishafuzu, ikiiacha Coton Sport na Al Hilal kupigania nafasi ya pili wakati Raja Casablanca itakamilisha mkiani.