Wengi waunga mkono taifa la Palestine

Kura ya maoni iliyoendeshwa na BBC imeonyesha kwamba idadi kubwa ya watu duniani wanaunga mkono Palestine kujiunga na Umoja wa mataifa kama taifa huru.

Haki miliki ya picha AP
Image caption watu wengi duniani wanataka Palestine itambuliwe kama taifa huru

Aidha wengi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanaunga mkono taifa jipya la Palestine kuundwa chini ya mipaka iliyokuwepo kati yake na Israel kabla ya vita vya mwaka 1967.

Taarifa zinasema Wapalestine wamelenga kutumia uungwaji mkono huu kushinikiza kutambuliwa kama taifa mpya katika mkutano mkuu wa Umoja wa mataifa unaofanyika wiki hii mjini New York Marekani.

Mwandishi wa BBC Barbara Plett anasema

Kuna masuala mengine ambayo yanaungwa mkono kwa kiasi kikubwa katika umoja wa mataifa kuliko suala la kuwepo kwa taifa huru la kipalestina kuambatana na mipaka iliyochorwa mwaka wa sitini na saba.

Umoja wa mataifa umeidhinisha maazimio kadhaa yanayoungwa mkono uhuru wa Palestina, lakini umoja huo umeachia jukumu la kutafuta muafaka na Israel katika mazungumzo yanayoongozwa na marekani.

Lakini kwa kuwa mazungumzo hayo yamesambaratika, Palestina sasa imegeukia umoja wa mataifa, ikitaka kutambuliwa kama mwanachama kamili wa umoja huo.

Pendekezo hilo ni sharti liidhinishwe na baraza la usalama la umoja wa mataifa hatua inayoonekana kuwa haitafanikiwa. Marekani imetangaza kuwa itaipigia kura ya turufu pendekezo kama hilo.

Pamoja na mshirika wake Israel, marekani imesisitiza kuwa njia ya pekee ya palestina kutambuliwa kama taifa huru ni kupitia njia ya mazungumzo ya moja kwa moja, na kuwa mbinu yoyote ya kushinikiza umoja wa mataifa huenda ikahujumu kurejelewa kwa mazungumzo hayo.

Lakini wakosoaji wakiwemo wanachama wa vugu vugu la Hamas ambalo linathibiti eneo la Gaza, wanasema hatua hiyo ni njama ya kisiasa na mpango wa kuligawanya taifa hilo.

Uhasama mkali unatarajiwa kati ya Kundi hilo la Hamas na hasimu wake Fatah linaloongozwa na rais Mahmoud abbas.

Ikiwa Abbas atarajea bila chochote kutoka kwa mkutano huo wa umoja wa mataifa utakaofanyika mjini New York, huenda akapoteza imani na kundi hilo la Hamas.