Dereva wa CARE atekwa kambini Kenya

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wakimbizi wa Somalia kambini Daadab

Dereva mmoja wa shirika la misaada la CARE hajulikani alipo baada ya kutekwa kwa mtutu wa bunduki kwenye kambi ya wakimbizi karibu na mpaka wa Somalia na Kenya.

Shirika la Care nchini Kenya limesema watu watatu waliingia katika gari hilo Jumatatu na kumwamuru dereva kukaa nyuma ya gari na kuondoka nalo.

Utekaji nyara huo umetokea karibu na Dadaab – kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Care limepunguza juhudi zake za misaada kufuatia tukio hili la kwanza la kushambuliwa kwa mfanyakazi wake tangu kutangazwa kwa baa la njaa katika shemu kadhaa za Somalia mwezi Julai.

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 1,000 wanangia kila siku katika kambi ya Dadaab wakikimbia njaa na vita.

Makumi elfu ya watu wamekufa kwa kile Umoja wa Mataifa unakiita ukame mbaya kuwahi kutokea katika eneo hilo katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

Miaka 20 ya mapigano na ukosefu wa serikali ya kitaifa inaifanya Somalia kuwa eneo lililoathirika zaidi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa CARE nchini Kenya, Gary McGurk, utekaji nyara huo ulitokea mchana kweupe.

Haijajulikana watekaji nyara hao walitoka nchi gani au walikolipeleka gari hilo na dereva.

"Tumesitisha mpango wetu wa misaada [Daadab] isipokuwa ile ya kufa na kupona," Bw McGurk aliiambia BBC.

Care linasema bado linasambaza maji na chakula lakini limesitisha huduma za elimu na ushauri.

Mwandishi wa BBC Afrika Mashariki Will Ross anasema Hagadera, ambako utekaji nyara umetokea ni moja kati ya maeneo matatu yanayounda kambi ya Dadaab, ambayo kwa sasa inafahamika kama mji mkubwa wa tatu nchini Kenya na ina nyumba karibu 450,000 za wakimbizi

Ukosefu wa usalama ni ni tatizo kubwa na ripoti zinasema ubakaji ni kawaida ,anasema.

Mapema mwezi huu Mwingereza mmoja aliuawa na mkewe kutekwa nyara eneo la kusini katika mpaka wa Somalia na Kenya. Inaaminika sasa kuwa anashikiliwa na kundi la maharamia.

Umoja wa Mataifa unasema inagharamia ili vituo vingi vya polisi viwekwe na matumaini ya usalama kurejea wakati vituo vipya vya ukaguzi vitakapowekwa mpakani Somalia.

Maeneo sita ya Somalia yanametangazwa kuwa yana janga la njaa sehemu kubwa ya kusini ikidhibitiwa na kundi la kiislam la al-Shabaab.

Kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaeda-limepiga marufuku mashirika mengi ya misaada katika eneo lake tangu miaka miwili iliyopita.