Wapiganaji wanasonga mbele Sirte

Wapiganaji wa Halmashauri ya Mpito ya Taifa ya Libya, wanaendelea kusonga mbele ndani ya mji wa Sirte, alikozaliwa Kanali Gaddafi.

Haki miliki ya picha Reuters

Baada ya mapigano kukwama kwa siku kadha, jeshi la Kanali Gaddafi limesukumwa nyuma, katika vitongoje vya mashariki mwa mji wa Sirte, na wapiganaji wa serikali ya muda wanasonga mbele kuelekea kati ya mji.

Wanajeshi waliobaki wa Gaddafi walijaribu kuzuwia shambulio, lakini silaha kubwa na shime iko upande wa wapiganaji.

Na makamanda wao wanaamini kuwa wataiteka Sirte karibuni.

Tayari kuna mapigano upande wa magharibi wa mji wenyewe, na vifaru na bunduki kubwa upande huo zinaendelea kusonga mbele, na kuuzingira mji.

Taarifa za wale walioukimbia mji zinaeleza kuwa wakaazi wengi wa Sirte hawajui kuwa mji mkuu, Tripoli, tayari umeshatekwa, kwa sababu ya propaganda wanayoambiwa.

Na wana wasiwasi ikiwa wapiganaji wanakuja kuwakomboa au kuwatesa.

Hatima sasa inategemea nguvu za wanajeshi wa Gaddafi, ambayo itaamua kama vita vitamalizika haraka au vitaishia kuwa mapambano ya barabarani kutoka nyumba hadi nyumba.