Rooney kukaa nje zaidi ya wiki, aumia

Wayne Rooney atakosa kuwemo kwenye kikosi cha Manchester United kwa mechi mbili zijazo, kwa mujibu wa meneja Sir Alex Ferguson, anayeamini mchezaji huyo "atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki moja".

Haki miliki ya picha ap
Image caption Wayne Rooney

Mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya England, hakucheza mechi waliyotoka sare ya bhao 1-1 dhidi ya Stoke siku ya Jumamosi, baada ya kupata maumivu ya msuli wa paja wakati akifanya mazoezi siku ya Ijumaa.

Manchester United siku ya Jumanne wataingia uwanjani kuikabili Basel katika hekaheka za Ubingwa wa Ulaya, kabla ya kuwakaribisha Norwich City wiki ijayo.

Kwa mujibu wa Ferguson, Rooney hakuumia sana na hafikirii kama ataweza kuwa tayari kucheza wiki ijayo.

Rooney huenda pia akakosa kucheza mechi ya kufuzu kwa mashindano ya Euro 2012 wakati England itakapoikabili Montenegro tarehe 7 mwezi wa Oktoba, iwapo hataweza kucheza mechi mbili za Manchester United kabla ya Fabio Capello hajatangaza kikosi chake.

Hali hiyo itakuwa pigo kwa Manchester United wanaoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya England, ambao pia walimkosa mlinzi Jonny Evans aliyeumia wakati akipiga jaramba na pia mshambuliaji Javier Hernandez aliyelazimika kutoka katika dakika ya 11 katika mechi na Stoke baada ya mguu wake kufa ganzi.