Wenger aonya uchumi kuathiri soka

Arsene Wenger amekiri kiwango cha chini cha soka kwa timu yake ya Arsenal kilichangia kupungua kwa mashabiki wake uwanjani wakati timu hiyo ilipocheza na Bolton siku ya Jumamosi.

Image caption Arsene Wenger

Lakini meneja huyo wa Arsenal ameonya kwamba mdororo wa uchumi unaoelekea kuikumba dunia huenda ukasababisha pia mashabiki kupungua katika viwanja mbalimbali vya soka England.

"Kwanza tulikuwa na matokeo mabaya hivi karibuni na pili ni ukweli tunaelekea katika matatizo ya uchumi", alisema Wenger.

"Viwanja vitakabiliwa na upungufu wa watazamaji haraka sana na tayari hilo tumeanza kuliona."

Maeneo yaliyokuwa na vitu vitupu yalionekana kwa urahisi wakati Arsenal walipoilaza Bolton mabao 3-0 katika uwanja wa Emirates, Robin van Persie akifunga mabao mawili na bao la tatu likipachikwa na Alex Song dakika za mwisho

Na wenger akaongeza kusema: "Na bado tutakabiliwa na matatizo zaidi na nadhani soka nayo inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi pia.

"Unaweza kuona vilabu vyote vya England na vile vya Ligi Kuu watu wanapungua kila siku kwenda uwanjani. Pengine sisi hali yetu ni tofauti kwa vile tumeanza vibaya ligi, lakini vilabu vingine pia vinakabiliwa na matatizo kama hayo."

Mashabiki wa Arsenal wanalazimika kulipa kiwango kikubwa cha tikiti kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya England, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kitengo cha bei za tikiti za michezo cha BBC mwanzoni mwa msimu huu.

Hadi sasa mahudhurio katika mechi za Ligi Kuu ya England yanaonekana kutotetereka, lakini baadhi ya vilabu vimecheza mechi tatu tu katika viwanja vyao vya nyumbani.