Benki ya Dunia yaongeza fedha za Ukame

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mama wa Kisomali akiwa na mtoto wake mwenye utapiamlo

Benki ya Dunia imetangaza kuongeza fedha karibu kiasi cha dola bilioni 2 kwa ajili ya ukame katika Pembe ya Afrika.

Benki hiyo imesema fehda hizo zinahitajika kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu.

Benki ya Dunia inasema nchi katika ukanda huo zinakabiliana na ukame mbaya kuwahi kutokea kwa zaidi ya nusu karne sasa.

Hali hiyo, Benki inasema, inasababisha kuongezeka kwa utapiamlo na ukosefu wa usalama wa chakula na kufanya wengi kukimbia makazi yao.

Kwa miaka ijayo, Benki hiyo itatoa kiasi cha dola 1.8 bilioni (sawa na £1.2 bilioni ) kusaidia karibu mara nne ya kiasi kilichoahidiwa mwezi Julai.

Lakini imesema bado kuna upungufu wa kiasi cha dola bilioni moja kinachotakiwa kutolewa kwa watu milioni 13 ambao wanahitaji Kenya, Ethiopia, Eritrea na Somalia.

Kutoa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Somalia inabaki kuwa changamoto kubwa kwa sababu ya migogoro ya ndani ya nchi na kupanda kwa bei ya chakula, Mwandishi wa BBC Marcus George anaripoti kutoka Washington.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 10,000 wamekufa katika ukanda huo na tatizo hilo linaweza kuwa kubwa zaidi katika wiki zijazo.