Robin van Persie hana haraka na mkataba

Mshambuliaji wa Arsenal, Robin van Persie amesema hana haraka kuahidi chochote kwa mustakabal wa mkataba wake mrefu katika klabu hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Robin van Persie

Van Persie mwenye umri wa miaka 28 nahodha wa Arsenal msimu huu, amebakiza miaka miwli kabla mkataba wake haujamalizika.

Inafahamika Robin anataka kuhakikishiwa na meneja wake Arsene Wenger juu ya malengo ya klabu, kufuatia kuuzwa hivi karibuni kwa Cesc Fabregas na Samir Nasri.

"Sidhani kama ni jambo la busara kuzungumzia mambo hayo wakati msimu ukiwa unaendelea," Van Persie alinukuliwa na magazeti kadha.

Naamini unatakiwa kuwa na wakati muafaka wa kukaa kitako na kuzungumzia masuala yanayokuhusu.

"Si kwangu mimi tu, ni suala linalohusu timu. Hatuzungumzii kwa wakati huu kwa sababu tupo katika pirika nyingi - tunacheza mechi kila baada ya siku tatu au nne.

"Bado nina karibu miaka miwili katika mkataba wangu, kwa hiyo kwa wakati huu mambo yote ni shwari. Lakini siwezi kujua, tutaangalia baadae.

"Sina matatizo na mkataba wangu , nipo vizuri. Ndivyo mambo yalivyo, siwezi kusema mengi zaidi. Nitaangalia baadae mustakabali utakavyokuwa."

Iwapo Van Persie atakuwa mgumu kumwaga wino kwa mkataba mpya, Arsenal inaweza ikakabiliwa na matatizo sawa na yaliyoletwa na Nasri, aliyegoma kurefusha mkataba wake mwishoni mwa msimu na baadae akauzwa kwa Manchester City.

Kumpoteza Van Persie, aliyekwishafikisha mabao 100 kwa Arsenal baada ya kufunga mabao mawili siku ya Jumamosi, waliposhinda mabao 3-0 dhidi ya Bolton na yeye ni mchezaji muhimu kwa Arsenal, litakuwa ni pigo jingine kubwa kwa klabu hiyo.

Wenger amekwishaeleza hayo baada ya kutoa tamko katika mtandao rasmi wa Arsenal sababu zilizomfanya amkabidhi mshambuliaji huyo jukumu la unahodha msimu huu.

"Nadhani ana mtazamo mzuri wa uongozi uwanjani," alisema Wenger. "Kiufundi ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu na anaheshimika na wachezaji wenzake. Na sasa ameongeza eneo la pili nalo kuzungumzia mawazo yake. Ina maana unapata heshima fulani.