Mazungumzo yafanyika kuepusha ghasia uchaguzi DRC

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Joseph Kabila

Vyama vikubwa vya upinzani nchini DRC vimeanza mazungumzo ya siku mbiliyenye lengo la kudhibiti ghasia wakati wa uchaguzi mwaka huu.

Uchaguzi wa Rais utafanyika Novemba 28 , uchaguzi kwa miaka ya nyuma umekuwa ukikumbwa na migogoro ambayo imegharimu maisha ya watu.

Wajumbe wako mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kwa mazungumzo yaliyoandaliwa na Umoja wa Afrika na Taasisi ya Amani na Mafunzo ya Usalama.

Uchaguzi umekuwa ukiathiriwa na madai ya udanganyifu wa kura.

Mapema mwezi huu, polisi walitumia mabomu ya machozi kutawanya mamia ya wafuasi wa upinzani ambao waliandamana mpaka ofisi za Tume ya uchaguzi kupinga madai ya wizi wa kura.

Vyama vya upinzani vimekosoa mabadiliko katika mfumo wa upigaji kura unaolenga kumchagua Rais bila duru ya pili utaratibu unaompendelea Rais wa sasa Joseph Kabila.

Serikali inasema inataka kuepuka kurudia migongano ambayo iliharibu duru ya pili ya uchaguzi ambao Bw Kabila alishinda na amekuwa madrakani tangu 2001.

Hata hivyo, mgombea kutoka upande wa upinzani Bw Etienne Tshisekedi, wa muungano wa vyama vya Union for Democracy na Social Progress, ametoa wito daftari la wapiga kura lifanyiwe ukaguzi.

Ghasia za hivi karibuni zimechangiwa na mvutano kati ya kundi la Bw Tshisekedi na wa wanachama kutoka chama cha Bw Kabila cha People's Party for Reconstruction and Democracy.