Fifa yaitaka Zimbabwe kutoa adhabu kali

Haki miliki ya picha Getty Images

Kiongozi wa usalama wa Fifa Chris Eaton, amekitaka chama cha soka cha Zimbabwe, kuwaadhibu vikali wachezaji na maafisa waliopatikana na hatia ya kupanga matokeo ya mechi.

Uchunguzi uliofanywa na Chama cha Soka cha Zimbabwe (Zifa) kutokana na ziara ya timu ya taifa iliyofanya bara Asia kati ya mwaka 2007 na 2009 na kugundua wachezaji walilipwa pesa kwa makusudi wapoteze mechi.

Eaton amesema anatazamia adhabu kali itatolewa kulingana na makosa yenyewe.

Chris Eaton aliidhinisha Zifa iunde tume huru ya nidhamu iliyoongozwa na jaji mstaafu ambayo itatoa adhabu kwa makosa yanayohusiana na soka.

Zifa ina matumaini tume hiyo itakamilisha kazi yake mwishoni mwa mwaka.

"Iwapo uamuzi utahusisha adhabu, nitaiomba kamati ya nidhamu ya Fifa kufikiria adhabu itakayohusisha dunia nzima" Eaton alikiambia kitengo cha michezo cha BBC.

Lakini pia ameshauri kuna uwezekano kwa baadhi ya wachezaji watahurumiwa.

Polisi wa Zimbabwe watafanya kazi pamoja na shirika la polisi la kimataifa - Interpol kupambana na masuala ya uhalifu na tume ya serikali ya kupambana na rushwa nchini Zimbabwe pia itahusishwa.