Ferguson awaita wachezaji wake "wazembe"

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson, ameshutumu kikosi chake kwa kuonesha "uzembe" baada ya kuongoza kwa mabao mawili na baadae wakawa na kibarua kigumu cha kusawazisha na kufanikiwa kwenda sare ya 3-3 dhidi ya timu ya Basel katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika uwanja wa Old Trafford.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sir Alex Ferguson

Manchester United walikuwa wanakabiliwa na hatari ya kupoteza mchezo katika uwanja wao kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi 17 hadi pale Ashley Young aliposawazisha kwa kichwa dakika za mwisho na kufanikiwa kupata pointi moja ambapo ngome yao ilipwaya sana.

Ferguson amesema: "Nadhani tulikuwa wazembe kwa kiasi fulani. Safu yetu ya ushambuliaji ilicheza vizuri na kulikuwa na wakati tulicheza vizuri sana, hasa kipindi cha kwanza.

"Uzembe huo umetugharimu, na Basel wangeweza kufunga mabao matatu kipindi cha kwanza. Labda unaweza kusema ni kuwakaribisha baadhi ya wachezaji katika mashindano ya ubingwa wa Ulaya kwa vile ni mara yao ya kwanza, lakini tulipwaya katika muda mwingi wa mchezo."