Prof Maathai kuzikwa kitaifa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Prof Wangari Maathai

Rais wa Kenya Mwai Kibaki ametangaza siku mbili za maombelezo kufuatia kifo cha Profesa Wangari Maathai.

Kulingana na taarifa ya rais Kibaki iliyotumwa kutoka Ikulu, hayati Profesa Maathai atafanyiwa mazishi yenye hadhi ya kitaifa.

Pia ametangaza siku mbili za kuomboleza kifo cha mwanaharakati huyo wa kutetea haki za mazingira.

Kuanzia kesho hadi Ijumaa bendera kote nchini Kenya zitapeperushwa nusu mlingoti.

Haya ndio yatakuwa mazishi ya kitaifa ya tatu kufanywa tangu Kenya ipate uhuru mwaka 1963.

Mazishi ya kwanza yalifanyika mwaka 1978 baada ya kifo cha rais mwanzilishi wa Kenya Jomo Kenyatta na mara ya pili ni baada ya kifo cha makamu wa rais Michael Kijana Wamalwa.

Tofauti na viongozi hawa Profesa Maathai hakuwa kiongozi wa serikali wakati wa kifo chake.

Awali taarifa kutoka familia ya mwanaharakati huyo ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya amani ya Nobel, ilisema bado wanajadiliana kuhusu siku ya maziko na eneo gani.

Profesa Maathai alifariki Jumapili usiku baada ya kuugua saratani ya uzazi.

Viongozi wamekuwa wakituma salamu zao za rambirambi kutoka pembe zote duniani.