Ujerumani yarejesha mafuvu ya Namibia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mafuvu ya Wanamibia

Ujerumani imerejesha mafuvu ya Wanambia ishirini waliofariki dunia baada ya fujo dhidi ya utawala wa ukoloni wa Kijerumani zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Wanamibia hao ni miongoni mwa mamia ya watu walioachwa na njaa hadi kufa baada ya kuwekwa kwenye makambi.

Baadhi ya waliokufa walikatwa vichwa vyao na kupelekwa Ujerumani, ikidhaniwa kufanyiwa utafiti wa kisayansi.

Katika miaka ya 1880, katika kile kilichojulikana kama kinyang'angayiro cha Afrika Ujerumani iliitwaa nchi ambayo siku hizi inajulikana kama Namibia na wakaiita Kusini Magharibi ya Afrika ya Ujerumani.

Lakini mnamo mwaka 1904 Waherero wanaowakilisha kundi kubwa la makabila 200 hivi waliasi dhidi ya utawala wa kikoloni na kuwaua zaidi ya raia 120.

Wajerumani walijibiza kwa ukatili mkubwa.

Jenerali Lothar Von Trotha alitia saini amri ya kuwaaangamiza Waherero na kuwashinda katika vita vya Waterberg na kuwatimua hadi jangwani ambako wengi wao walikufa kutokana na kiu.

Ni Waherero 15,000 tu walinusurukia katia ya 65,000 waliokuwepo.

Inaaminika watu 10,000 wa kabila la Nama pia waliuwawa.

Wale waliokimbia mapigano walizuiliwa wasirejee kutoka jangwa la Namib na kufuatiwa na njaa.

Baadhi ya taarifa pia zililishtumu jeshi la Ujerumani kwa makusudi kumwaga sumu katika visima vya jangwani.

Baadae wafungwa walitokomezwa katika kambi za mateso na kazi ngumu.

Mwaka 1985, ripoti ya Umoja wa mataifa ilielezea matukio hayo kuwa ni njama ya kuwaangamiza kabisa watu wa kabila la Herero na Nama na kuelezea kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20.

Mnamo mwaka 2004 balozi wa Ujerumani nchini Namibia alielezea masikitiko yake, lakini serikali ya Ujerumani imesema haitawalipa fidia jamaa za waathiriwa.