Sunderland yamsimamisha Bramble

Klabu ya mpira inayocheza katika Ligi kuu ya England, Sunderland, imemsimamisha beki wake Titus Bramble baada ya mchezaji huyo kukamatwa akishukiwa kuwa na dawa ya kuongezea nguvu pamoja na kosa la ubakaji.

Image caption Titus Bramble

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ambaye hapo zamani alichezea klabu ya Newcastle na Wigan alihojiwa kabla ya kuachiliwa kwa dhamana hapo jana.

Taarifa ya klabu imesema kuwa: "Titus Bramble amesimamishwa wakati majibu ya upelelezi yakisubiriwa.

Taarifa hiyo imeongezea kusema kuwa "mchezaji huyo hatoshiriki mazowezi ya timu au kuwa tayari kuchaguliwa kwa ajili ya kushiriki mechi yoyote kwa wakati huu."

Titus Bramble alianza kucheza soka katika klabu ya mji alikozaliwa wa Ipswich, kabla ya kuhamia Newcastle United kwa kitita cha pauni milioni sita.

Baada ya hapo akajiunga na klabu ya Wigan Athletic kabla ya kurejea kaskazini mashariki alipojiunga na Sunderland mwaka uliopita.

Beki huyo aliyechaguliwa mara kumi kuichezea Timu ya vijana wa England wenye umri ulio chini ya miaka 21, alishiriuki mchuano wa klabu yake ilipofungwa na Norwich 2-1 mnamo siku ya jumatatu.