Maelfu waukimbia mji wa Sirte

Mtiririko wa raia wa Libya wanaoukimbia mji wa Sirte ulionekana huku wamebeba mali zao kwenye magari.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raia wakimbia mji wa Sirte

Wakuu wa vikosi vya waasi wanaotawala nchi hiyo wamesema kua wanatii mapatano ya kusitisha mapigano ili kuruhusu raia waondoke, kabla ya shambulio lao la mwisho.

Huku nyuma kundi kutoka shirika la mwezi mwekundu limeruhusiwa kuingia mji wa Sirte ambako linasema huduma ya afya inahitajika.

Sirte ni mojapo ya miji muhimu ambayo bado inapinga utawala wa waasi. Bado Kanali Gaddafi hajulikani alipo.

Gari ndogo, mabasi na malori yaliyojaa mizigo ya nyumbani yalisimama kwenye vizuizi vya wapiganaji wa utawala wa NTC nje kidogo mwa mji wa Sirte.

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Usitishaji mapigano ni kuruhusu raia waondoke

Raia hao wanaokimbia wameielezea hali katika mji kuwa mbaya kiasi kwamba chakula kimepungua, maji na umeme pia ni shida.

Mwanamume mmoja, Ali, amesema kua familia yake inakimbia kwa sababu wamejikuta katikati ya mashambulizi ya mabomu yanayodondoshwa na ndege za Nato pamoja na milipuko inayorushwa na waasi.

Shirika la mwezi mwekundu lenye makao yake makuu mjini Geneva linasema hadi watu 10,000 hadi sasa wameondoka mji wa Sirte, huku theluthi ikiweka kambi yake katika maeneo ya jangwa kilomita chache kutoka mji wa Sirte karibu na nyumbani kwao.

Shirika hilo linasema kua hospitali kuu ya mji huo imezidiwa na watu wanakufa kila uchao kutokana na kupunguliwa na pumzi na mafuta.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Huduma ya afya shida Sirte