Wydad yailaza Enyimba nusu fainali

Bao la Pascal Angan dakika za mwisho limeipatia ushindi timu ya Moroccan ya Wydad Casablanca 1-0 dhidi ya Enyimba ya Nigeria katika mechi ya mzunguko wa kwanza nusu fainali ya Ubingwa wa Afrika siku ya Jumamosi.

Image caption Nembo ya Enyimba

Mshambuliji huyo wa kimataifa wa Benin alifunga bao hilo kwa kichwa katika dakika ya 89 mjini Casablanca.

Timu hiyo ya Wydad tayari ilikwishakata tamaa kupata ushindi dhidi ya ngome ngumu ya Wanigeria hao hadi dakika ya 89 walipopata adhabu ya mkwaju wa moja kwa moja.

Inakuwa ni mara ya kwanza kwa mabingwa hao mara mbili wa Afrika Enyimba, kupoteza mchezo katika mashindano muhimu mwaka huu baada ya kushinda mara nane na kutoka sare mara tatu, ikiwemo moja dhidi ya Raja wakati wa mechi ya ufunguzi wa makundi katika uwanja huo huo wa Casablanca.

Enyimba itaikaribisha Wydad katika mechi ya marudiano tarehe 16 mwezi huu wa Oktoba katika mji wa Aba kusini - mashariki mwa Nigeria, huku Wydad mabingwa wa Afrika mwaka 1992 wakiwania kupata bao la ugenini ambalo litawaacha wapinzani wao wawe na kibarua kigumu cha kufunga mabao matatu ili waweze kufuzu katika fainali itakayochezwa mwezi wa Novemba.