19 wauawa katika kijiji Nigeria

Image caption Waathirika wa mashambulio kaskazini mwa Nigeria

Takriban watu 19 wamepigwa risasi au kukatwa kwa mapanga katika tukio baya zaidi kwenye kijiji kimoja kilichoko kaskazini magharibi mwa Nigeria, polisi wamesema.

Walioushuhudia wanasema watu karibu 150 walivamia kijiji cha Lingyado, katika jimbo la Zamfara karibu na mpaka wa Nigeria na Niger, wakiwa na bunduki na mapanga.

Msemaji wa polisi anasema inaonekana kama ni uvamizi wa kulipiza kisasi kufuatia uvamizi kama huo mwezi wa nane.

Maafisa wa usalama wako katika eneo hilo kujaribu kutuliza hali.

Msemaji wa polisi Sunusi Amiru anasema watu wengine sita walijeruhiwa katika uvamizi huo na kwa sasa wanatibiwa.

" Tuko imara kabisa, na tunawasaka washukiwa, tumepeleka maafisa zaidi kwenye maeneo yaliyo hatari zaidi," aliambia shirika la habari la Reuters.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria Jonah Fisher anasema walioathirika walivamiwa wakati wakitoka nje ya nyumba zao.