Shambulio baya latokea Somalia

Image caption Mlipuko Somalia

Takriban watu 55 wameuawa na kinachodhaniwa kuwa mlipuko mkubwa uliofanywa na mtu aliyejitoa mhanga karibu na jengo la serikali kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Walioshuhudia wamesema lori lililokuwa na milipuko lilikwenda moja kwa moja kwenye lango karibu na wizara moja ya serikali na kulipua.

Sheikh Ali Mohamed Rage, msemaji wa kundi la wanamgambo la al-Shabab, aliiambia BBC kuwa wamehusika kwenye shambulio hilo.

Mwandishi wa BBC alisema eneo kuu la jengo hilo liliharibiwa.

Mwandishi wa BBC wa Somalia Mohammed Dore alisema magari yalikuwa yamechomwa moto, miili ilionekana ikiwa imezagaa mitaani na askari waliopata mshtuko walikuwa wakifyatua risasi ovyo.

Mwandishi wetu alisema, miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa ni wanafunzi waliokuwa wamepanga foleni katika lango kuu kufanya mtihani katika wizara ya elimu ili kupata ufadhili wa kusoma Uturuki.

Alisema ni tukio baya zaidi yeye binafsi kushuhudia.

Viongozi wa serikali ya mipto inayodhaminiwa na umoja wa mataifa walikuwa wakikutana kwenye jengo hilo wakati shambulio hilo lilipotokea.

Hata hivyo, bado haiko wazi iwapo ni miongoni mwa waliofariki dunia.

Afisa mmoja kutoka Umoja wa Afrika, yenye majeshi yake ya kutunza amani Somalia, alisema tukio hilo "ni la hatari sana".