Hatari ya mpango wa uzazi

Image caption Sindano: Maarufu kwa kupanga uzazi

Wanasayansi wanadai kuwa aina moja ya dawa ya kupanga uzazi maarufu miongoni mwa wanawake katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kusini inawaweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa maradhi ya ukimwi.

Utafiti huu ulifanywa miongoni mwa watu walio kwenye ndoa elfu nne katika mataifa kadhaa barani Afrika na kubainika kuwa wanawake wanaotumia sindano yenye homoni kupanga uzazi wako katika hatari maradufu ya kuambukizwa virusi vya HIV na kuvisambaza kwa waume zao.

Wanasayansi hao wamechapisha matokeo yao katika jarida la kimatibabu la Lancet.

Wanapendekeza matumizi ya mipira au kondom kama kinga zaidi dhidi ya maradhi ya Ukimwi.

Hata hivyo inasemekana matokeo haya huenda yatatoa changamoto katika utoaji wa huduma za afya kwani sindano hiyo ni rahisi kutumika, ina bei nafuu, hutumika kwa muda mrefu na pia inawasadia maelfu ya wanawake kujinga dhidi ya maradhi na hata vifo wakati wanapopata mimba isiyotarajiwa.