Mlinda mlango Togo akasirishwa na kebehi

Emanuel Adebayor Haki miliki ya picha PA
Image caption Emanuel Adebayor

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya kandanda ya Togo, ambaye alipigwa risasi hali iliyosababisha asiweze tena kucheza soka, amewataka mashabiki wenye hatia ya kuimba maneno ya dhihaka dhidi ya Emanuel Adebayor wakati Tottenham ilipopambana na Arsenal waadhibiwe.

Mshambuliaji wa Tottenham Emmanuel Adebayor aliimbiwa nyimbo hizo za dhihaka na baadhi ya mashabiki wa Arsenal zilizokuwa zikihusu timu ya Togo iliposhambuliwa kabla ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010.

"Kwa kuimba nyimbo za dhihaka kama zile inaonesha kama vile wanashabikia ugaidi," Kodjovi Obilale alisema.

"Niliumizwa katika shambulio lile ndani ya basi. Wote waliodhihaki wanatakiwa kuadhibiwa vikali."

Aliendelea kusema: "Ni jambo baya sana, wamekwenda mbali sana na dhihaka zao. Watu wamepoteza maisha yao. Tunazungumzia suala la maisha kupotea. Sifahamu nini kibaya ambacho Adebayor amefanya. Yeye anacheza kandanda basi."

Obilale alipigwa risasi mbili mgongoni wakati wa shambulio la bunduki za rashasha lililoelekezwa katika basi la timu ya taifa ya Togo walipokuwa wakivuka mpaka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuingia Angola tarehe 8 mwezi wa Januari mwaka 2010, siku mbili kabla ya kuanza mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Watu wawili waliokuwa katika msafara wa timu ya Togo waliuawa katika shambulio hilo.

Tottenham imeahidi kuwafungia kuingia uwanjani kwao mashabiki watakaopatikana na hati ya kuimba nyimbo hizo za dhihaka wakati wa mechi kati yao na Arsenal.

Meneja wa Spurs Harry Redknapp na mwenzake wa Arsenal Arsene Wenger kwa pamoja wamelaani dhihaka hizo za mashabiki wakati Spurs iliposhinda mabao 2-1.