ANC yapinga matamshi ya Desmond Tutu

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Askofu Desmond Tutu na Dalai Lama

Chama tawala cha Afrika Kusini ANC kimetupilia mbali madai ya Askofu Desmond Tutu kuwa chama hicho " ni kibaya kuliko serikali ya enzi za ubaguzi wa rangi".

Matamshi ya mshindi huyo wa tuzo ya Nobel yalitolewa baada ya Dalai Lama kufuta safari yake ya Afrika kusini baada ya serikali hiyo kushindwa kumpa viza wakati unaotakiwa.

Kiongozi wa kiroho wa Tibet alitakiwa kushiriki sherehe za kuadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwa askofu huyo siku ya Ijumaa.

Taarifa ya ANC ilisema, " Tunatoa wito kwa askofu apunguze hamaki."

Pretoria imeshikilia msimamo wake kuwa haikushinikizwa na China kuzuia safari hiyo.

Dalai Lama

Dalai Lama amefutilia mbali ziara yake ya Afrika Kusini ambapo alikuwa amealikwa na mshindi mwenzake wa tuzo ya amani ya Noble Askofu Mkuu Desmond Tutu.

Ofisi ya kiongozi huyo wa kidini kutoka Tibet imesema serikali ya Afrika Kusini imekosa kumpa visa, yaani kibali cha kuingia nchini humo kwa wakati.

Alitarajiwa kuhudhuria sherehe za Ijumaa za kuadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa Askofu Tutu.

Kwa upande wake serikali ya Afrika Kusini inasema haikushinikizwa na Uchina kumzuia Dalai Lama kuizuru nchi hiyo .

Mzozo huu ulizidi kutokota pale Naibu Rais wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe alipofanya ziara ya siku nne nchini Uchina na kufanya mazungumzo pamoja na kutia saini mikataba kadhaa ya uhusiano wa kibiashara na uwekezaji.

Hakuzungumzia suala la visa alipokuwa Uchina.