BBC Swahili kuwa na mabadiliko

BBC Swahili Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ukurasa wa Swahili utafanana na kusara nyingine za BBC

Wavuti wa BBC Idhaa ya Kiswahili unafanyiwa mabadiliko makubwa, ambayo yataleta wepesi katika kurambaza na kuwa na muonekano wa kuvutia. Katika kipindi hiki utaona mabadiliko katika violezo [templates] vya baadhi ya kurasa za taarifa. Kutokana na hilo huenda ukashuhudia kutolingana katika muonekano na vitufe vya muongozo. Hata hivyo, maudhui yatasalia vile vile, ikiwemo taarifa mbalimbali, makala, sauti na video zitaendelea kuwepo.

Nini manufaa ya mabadiliko haya?

Muonekano mpya: Nafasi zaidi kwa ajili ya taarifa na habari mbalimbali za kila siku, pamoja na video na picha. Tutakuwa na uwezo wa kuonesha katika ukurasa wa mbele iwapo habari kuu zina habari nyingine zinazohusiana.

Maelekezo rahisi: Uoneshaji rahisi wa maudhui mbalimbali na hivyo taarifa, habari picha au video zitakuwa na wepesi kuzipata na kuziona.

Kurasa za habari: Kurasa za habari zitakuwa na muundo ambao mara utakapowasili katika wavuti unapata nafasi na kuona habari motomoto zilizopo ndani ya wavuti. Kiungo cha taarifa zinazohusiana kitakuwa ndani ya ukurasa wa taarifa inayosomwa au chini kabisa ya ukurasa.

Video: Kicheza video kitakuwa kikubwa na kitarusha video zenye ubora. Katika ukurasa wa sauti na video kutakuwa na kiungo cha kutazama video zaidi. Kwa njia hii, wale wanaotaka kutazama yaliyomo kwenye medianuai hawatalazimika kwenda katika maeneo mengine ya wavuti.

Mpya kabisa: Katika ukurasa wa mbele, taarifa mpya kabisa zitakuwa na tarehe na saa ambazo zimeandikwa au kubadilishwa.

Kusambaza: Kiungo ambacho kinaruhusu watumiaji kusambaza taarifa kwa marafiki zao kwa haraka na kwa urahisi kwa kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter.

Tafadhali tumia wasiliana nasi kutufahamisha iwapo umepata tatizo lolote wakati wa kipindi hiki cha mabadiliko.