Rais wa Liberia apata tuzo ya Nobel

Tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu imewaendea kina mama - rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, raia mwenzake wa Liberia Leymah Gbowee na Tawakkul Karman wa Yemen.

Haki miliki ya picha REUTERSLucas JacksonFiles
Image caption Mwanamke wa kwanza kuchaguliwa rais barani Afrika

Wanapata tuzo hiyo kutokana na mbinu zao za kuwatetea wanawake na haki za wanawake, pasipo kutumia nguvu, na kuimarisha nguzo mbalimbali za kijamii katika kupata amani.

Bi Johnson Sirleaf ni mwanamke wa kwanza barani Afrika aliyechaguliwa kama rais kuiongoza nchi yake, Bi Gbowee ni mtetezi wa masuala ya amani na Bi Karman ni mwanaharakati wa masuala ya kidemokrasia nchini Yemen.

"Nimefurahi sana kukabidhiwa tuzo", alielezea Karman, mwenye umri wa miaka 32, na mama aliye na watoto watatu, na ni mkuu wa kundi la wanawake la "Journalists without Chains", yaani waandishi wa kike wasiobanwa na vizuizi vyovyote katika kutekeleza kazi yao.

Amehusika sana katika kupanga maandamano ya kumpinga rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen.