Uganda yazimwa na Kenya

Mbio za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinakaribia tamati yake jumapili ambapo orodha ya Timu zitakazoshiriki itabainika baada ya mashabiki wa soka kushuhudia wikendi ya pata shika kwenye viwanja mbalimbali barani Afrika.

Image caption Black Stars yafuzu

Baada ya Timu zilizofuzu jumamosi bado kuna nafasi 10 za kuwaniwa katika michuano ya baadaye lero ikiwa ni pamoja na Taifa stars mjini Marakesh itakapozipiga na Morocco.

Hapo jana kwenye mechi iliyochezwa mjini Chingola, Zambia ilitoka sare na Libya na timu hizi mbili zikafuzu moja kwa moja.

Kabla ya mchuano huo Zambia ilihitaji pointi moja kufuzu il hali Libya ilihitaji isishindwe ili kusonga mbele.Zambia inamaliza ikiongoza kundi ikiwa na pointi 13 mbele ya Libya iliyo na pointi 12. Mechi nyingine ya kundi hilo la C Msumbiji iliirarua Comoro 3-0.

Faraja ya Tunisia ilipatikana kufuatia juhudi za Chad iliyoikatalia Malawi kwa kurudisha bao mnamo dakika za majeruhi. Hata hivyo Tunisia haikutegemea nguvu ya Chad pekee ikijitahidi na kuifunga Togo 2-0 mjini Tunis.

Mabingwa wa Afrika wa mwaka 2004 Tunisia walianza vizuri na katika kipindi cha kwanza Walid Hicheri akafungwa la kwanza kabla ya Saber Khelifa kuongezea la pili kipindi cha pili.

Tunisia inamaliza ya pili nyuma ya Botswana iliyomaliza kazi mapema ikiongoza kwa pointi 17 ,tunisia in pointi 14 na Malawi inaondolewa ikiwa na pointi 12. Matokeo ya jana yaliiona Nigeria ikimaliza 2-2 na Guinea na hivyo kuondolewa.

Ethiopia ikaichapa Madagascar 4-2, Zambia na Libya zikamaliza 0-0 lakini zote zinafuzu. Msumbiji ikaichapa Comorro 3-0

Angola siku ya Jumamosi iliweza kufuzu kuingia fainali za soka Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 katika mataifa ya Equatorial Guinea na Gabon, baada ya The Cranes ya Uganda, ikicheza na majirani Harambee Stars ya Kenya, kumaliza mechi yake Kampala kwa kutofungana mabao.

Wachezaji sita hivi walijiangusha chini uwanjani kwa kutoamini wameshindwa kupata ushindi katika mechi hiyo ili kufuzu, huku wengine walielekea chumba cha kubadilishia mavazi wakitiririkwa na machozi.

Baadhi ya mashabiki wa Uganda wanaamini kwamba kama mchezaji wa The Cranes David Obua, ambaye alifukuzwa kutoka kambi ya Uganda, kama angelicheza, pengine matokeo yangelikuwa tofauti.

Waliofurahi ni mashabiki wa Kenya, ambao walionekana wakiwa na mabango ambayo yaliwafanyia dhihaka, kama kuelezea "Ni kweli Uganda haijafanikiwa kufuzu kuingia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika miaka 34".

Katika viwanja vingine, Niger ilifuzu licha ya kufungwa magoli 3-0 na Misri.

Wapinzani katika kundi G, Afrika Kusini au Sierra Leone wangeliweza kufuzu, lakini katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Nelspruti, ilikwisha 0-0.

Nigeria pia ilishindwa kufuzu, baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Guinea katika mechi ya mjini Abuja.

Timu ya Syli Nationale imefuzu kwa kuongoza katika kundi B.