Sudan yatinga fainali

Morocco na Sudan zimekuwa nchi mbili zilizojaza nafasi zilizosalia kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Morocco ilifuzu kwa kuibwaga Tanzania 3-1 jumapili ikimaliza kileleni mwa kundi D mbele ya Jamhuri ya Afrika ya kati ambayo ilichapwa na Algeria 2-0.

Matokeo hayo yakamaanisha kuwa Sudan inajishindia nafasi iliyobaki ya mshindi wa pili bora kwa kumaliza vizuri nyuma ya Ghana katika kundi I.

Kwa bahati mbaya Jamhuri ya Afrika ya kati haikutimiza pointi za kutosha kuiondoa Sudan.

Mabao ya Morocco yalitiwa kimyani na Marouane Chamakh, Adel Taraabt na M'Bark Boussoufa katika mechi iliyochezwa mjini Marrakech - ambapo Taraabt aliingia dakika ya mwisho kufuatia mshambuliaji Youssf Hadji kujeruhiwa wakati akipasha viungo kabla ya mechi.

Image caption Cranes haikuwa na uhaba wa mashabiki Mandela

Kushiriki kwa Sudan kwa mara ya tatu mfululizo kwenye mashindano haya kunaifanya kuwa Timu pekee kutoka Kanda ya CECAFA baada ya Uganda, Kenya, Tanzania,Rwanda na Burundi kushindwa kufuzu.

Senegal iliendeleza rekodi yake ya kutofungwa katika michuano hii ya kuchuja Timu zitakazoshiriki fainali ya Kombe la Mataifa ikiishinda Mauritius 2-0.

Kwa upande mwingine Ivory Coast, ilikamilisha mechi zake za kufuzu na kuongoza kundi lake H kwa kuibwaga Burundi 2-1 mjini Abidjan.

Kolo Toure aliipatia Timu yake bao la kwanza mnamo dakika ya 77 baada ya Warundi kuonyesha kiburi cha kutotaka kufungwa, na dakika 9 baadaye Dugarry Nolabashinze akasawazisha bao la Kolo Toure.

Matumaini ya Burundi yalizimwa kwa bao la Yaya Toure katika dakika za majeruhi kuipa Ivory Coast ushindi wa 2-1.

Rwanda ilijishindia nafasi ya pili ya kundi hilo H kwa ushindi wa 1-0 nchini Benin.

Lilikua bao la Mere Kagere mnamo dakika ya sita lililobaini pande hizi mbili hadi mwisho wa pambano hili.

Michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya mwaka 2012 inaanza nchini Equatorial Guinea tareh 21 Januari, na mechi ya fainali ikitarajiwa katika mji mkuu wa Gabon, Libreville hapo tarehe 12 Febuari 2012.