Askofu wa Cantebury azuru Harare

Kiongozi wa kanisa la Kianglikana, Askofu wa Cantebury, Rowan Williams, amehubiri nchini Zimbabwe, akijaribu kupatanisha kwenye ugomvi kati ya Waanglikana nchini humo.

Akizungumza katika uwanja wa michezo wa taifa mjini Harare, Dakta Williams aliwasihi Wazimbabwe waache fujo.

Askofu aliyetengwa, Nolbert Kunonga, ambaye anamuunga mkono Rais Mugabe, ametuhumiwa kuwa anachochea fujo dhidi ya Wanglikana wasiokubaliana naye.

Dakta Williams ameomba kukutana na Rais Mugabe, na yuko katika safari ya nchi tatu za Afrika, pamoja na Malawi na Zambia.