Wapiganaji waingia mjini Sirte

Wapiganaji wa serikali ya mpito ya Libya wanasema wameteka lengo muhimu - jengo kubwa la ukumbi wa mikutano - katikati ya mji wa Sirte, ambako askari wengi walio wafuasi wa Gaddafi walikuwamo na kupigana vikali.

Haki miliki ya picha Reuters

Video moja inaonesha wapiganaji wakikaribia eneo hilo huku wakifyatua silaha zao, na huku wakijibanza kwenye kuta, na kisha kusonga mbele.

Kabla ya hapo wapiganaji waliteka eneo la chuo kikuu cha mji huo.

Kamanda wa wapiganaji anasema kuteka jengo la ukumbi huo kutafungua njia, kwa majeshi yake kuvamia mitaa ya kati ya mji.

Kuna wasiwasi mkubwa juu ya wakaazi walionasa katika mji wa Sirte.