Mapigano yasimama Sirte

Kumekuepo na mdororo mfupi katika mapigano ya Sirte nchini Libya wakati wapiganaji kutoka serikali mpya wakijikusanya baada ya siku yenye mtihani ya jana.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Askari wajipanga upya

Kusita huko kumewawezesha baadhi ya raia kutumia fursa hiyo kuuhama mji, lakini mwandishi wa BBC aliye nje kidogo ya mji anasema kua huenda askari wa Gaddafi nao wanajaribu kujipenyeza miongoni mwa raia wanaokimbia.

Huku vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Gaddafi vikiwa katika hali ya kuzidiwa ingawa vimejitolea kuulinda mji wa Sirte, wapiganaji wa utawala mpya wanakabiliwa na hali ngumu na kasi ya mwendo imepungua, licha ya kuwa vikosi vya Nato vilifanya mashambulizi kwenye maeneo kadhaa usiku kucha.

Kwenye barabara kuu mamiya ya raia wanakimbia vurumai ya mapigano. Magari yaliyojaa familia na mali zao yanaelekea magharibi mwa mji, mbali na medani ya vita.

Lakini kwenye kizuizi kilichopo nje ya Sirte kila gari linakaguliwa kabla ya kuendelea na safari.

Image caption Ukaguzi wa magari kutoka Sirte

Kuna shaka kwamba wapiganaji wengi wa upande wa Gaddafi, walioacha silaha zao na sare wamefichama ndani ya magari hayo wakijaribu kupenya kwa kisingizio kuwa ni raia.

Tumewaona wanaume kadhaa ambao waliamrishwa kuondoka kwenye magari na kuhojiwa nje ya vikwazo vya barabarani. Wengi hawakua na vibali na hadithi zao zilikua za kubabaisha. Wote walikana kuhusika katika mapigano, ingawa walionekana wamebabaika.