Misri yajitoa kuandaa kufuzu Olimpiki

Ghasia Cairo Misri Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ghasia Cairo Misri

Misri imejitoa kuandaa mashindano ya wanaume ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki kwa nchi za Afrika.

Mashindano hayo yanayoshirikisha timu nane ilikuwa yachezwe mjini Cairo kuanzia tarehe 26 mwezi wa Novemba hadi tarehe 10 Desemba, huku timu tatu zitakazomaliza nafasi ya juu zitafuzu kwa michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012.

Misri imethibitisha uamuzi wake huo kwa Shirikisho la Soka barani Afrika -Caf- kuhusu uamuzi wake huo, na kueleza sababu ni kutokana na uchaguzi wa bunge utakaofanyika hivi karibuni.

Kumekuwa na machafuko zaidi mjini Cairo katika siku za karibuni.

Pamoja na Misri, timu nyingine ni Algeria, Gabon, Ivory Coast, Morocco, Nigeria, Senegal na Afrika Kusini.

Shirikisho la Soka la Afrika- Caf - limeyafanya mashindano hayo kuwa ni ya kwanza kwa Afrika kushirikisha wachezaji chini ya umri wa miaka 23.

Bara la Afrika tayari lina mashindano mawili ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na miaka 20, ambapo timu tatu za juu zinafuzu kuwakilisha bara hilo katika fainali zinazoandaliwa na Fifa kwa umri wote huo.

Hadi sasa Caf haijasema lolote kuhusiana na uamuzi huo wa Misri.