Shirika la Amnesty lashutumu NTC Libya

Wafungwa Libya Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafungwa Libya

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa utawala wa muda wa Libya ukomeshe mtindo wa kuwakamata na kuwazuilia watu kiholela na vile vile kuwatesa wafungwa.

Katika ripoti yao shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema liligundua ushahidi unaoonesha kuwa maelfu ya wafungwa wamekuwa wakitesewa katika miezi hii michache iliyopita.

Waafrika kutoka kusini mwa jangwa la Sahara- yani Waafrika weusi wanaoshukiwa kuwa mamluki wa Kanali Gaddafi ndio walengwa wakuu, Baraza la Kitaifa la Mpito NTC limeahidi kuyaangalia madai hayo.

Na wakati huohuo kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mwanae Kanali Gaddafi, Mutassim Gaddafi amekamatwa.

Baadhi ya maafisa katika Baraza la Kitaifa la NTC wanasema kuwa alikamatwa katika mji wa Sirte ambao ni ngome ya familia ya Gaddafi.

Hatahivyo kamanda mmoja wa kijeshi amekanusha madai hayo ambayo yamepokewa katika miji mengine kwa shangwe na ufyatuaji risasi hewani.

Mwandishi wa BBC mjini Tripoli Caroline Hawley anasema kuwa ikithibitishwa kuwa Mutassim Gaddafi amekamatwa, hii itakuwa hatua kubwa kwa NTC.

Mutassim Gaddafi alikuwa ni afisa wa ngazi za juu katika jeshi la Kanali Gaddafi na pia alikuwa mshauri wa usalama wa kitaifa kwa baba yake.

Vikosi vya NTC vimesema vinadhibiti sehemu kubwa ya mji wa Sirte, lakini mwandishi wa BBC Wyre Davies aliye Sirte anasema vikosi hivyo vimerudishwa nyuma kidogo tangu siku ya Jumatano.

Shirika la Amnesty limechapisha ripoti yake yenye kichwa cha “ Mateso kwa wafungwa yanaichafua Libya mpya” baada ya kuwahoji wafungwa wapatao 300.

Shirika hilo lilitembelea magereza 11 ndani na nje ya Mji Mkuu Tripoli na katika miji ya Zawiya na Misrata kati ya tarehe 18 mwezi Agosti siku chache kabla ya mji wa Tripoli kukamatwa na tarehe 21 mwezi September.

Shirika hilo limesema limegundua utaratibu unaotumiwa kuwatesa watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Gaddafi ikiwa nipamoja na wanajeshi na watu wanaoshukiwa kuwa mamluki.