Mkutano wa viongozi wa Comesa

Jumuia ya Biashara ya Mashariki na kusini mwa Afrika, kwa kifupi, Comesa inaanza mkutano wa kilele wa siku mbili nchini Malawi.

Hata hivyo mkutano umegubikwa na mashaka juu ya waranti ya kimataifa ya kutaka Rais wa Sudan Bashir akamatwe.

Lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi ya kukuza sayansi na teknolojia katika mataifa 18 wanachama wa jumuia hiyo.

Lakini suala kuu linaloongoza mazungumzo kwa sasa ni mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari nchini Malawi na vilevile kama watii amri ya ICCile Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai ya kumkamata au kutomkamata Rais wa Sudan Hassan El Bashir kwa madai kuhusu uhalifu wa vitani.

Serikali ya Malawi imepuuza miito ya ICC kumkamata kiongozi huyo na badala yake amepokelewa kwa jamvi jekundu na ngoma za utamaduni wa nchi yao.

Suala jingine lenye utata kwenye mkutano huu ni mvutano katika mahusiano baina ya nchi jirani za Zambia na Malawi, Michael Sata, Rais mpya wa Zambia amesusia mkutano.

Serikali yake imeitaka Malawi imuombe radhi kiongozi huyo kwa kumkatalia kibali cha kuingia nchini humo mnamo mwaka 1997 alipokua kiongozi wa upinzani.

Wakati huo Bw.Sata alikamatwa kwenye mpaka wa Malawi na kuhojiwa kwenye kituo cha Polisi mjini Blantyre na baadaye kusafirishwa kwa gari hadi mpakani na kutupwa huko.

Suala jingine kwenye mkutano huu ni kwamba mwenyeji wa mkutano huu, Rais Bingu wa Mtharika alikua Katibu mkuu muasisi wa Jumuia ya Comesa miaka kumi na mitano iliyopita na kutimuliwa.

Sababu ya kumuondoa ikiwa kwamba hakuwa na mtazamo wa kuiwezesha jumuia hio kusonga mbele hata kuvuka kuingia karne mpya.

Lakini Dr Mutharika amekanusha madai hayo akisema kua sababu za kumuachisha kazi zilikuwa ni chagizo za kisiasa kutoka kwa wapinzani wake nchini Malawi na sio uwezo wake.

Leo anasimama kuwa Mwenyekiti wake.

Mbali na matatizo yaliyoukumba mkutano huo masuala yatakayojadiliwa ni pamoja na kujadili ni jinsi ya kutumia eneo lenye biashara huria kuimarisha biashara miongoni mwa wanachama.

Viongozi wa Mataifa watachunguza namna ya kuowanisha au kuondoa ushuru na vizuizi.

Kabla ya hapo mawaziri wa mashauri ya kigeni wa jumuia hiyo wamekua wakilalamika juu ya hali ya ukosefu wa sheria nchini Somalia, hali ambayo wamelaumu imesababisha Uharamia.

Walisema kua hali nchini Somalia ni tishio kuu kwa usalama siyo tu wa pembe ya Afrika bali Dunia nzima.

Viongozi wengine waliothibitisha kuhudhuria ni pamoja na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Nkuruziza wa Burundi, Isaias Aferweki wa Eritrea na Mfalme Mswati wa Swaziland. Mataifa mengine kama Kenya na Tanzania yanatuma wajumbe.