Mabenki yalalamikiwa duniani

Maandamano kupinga uroho wa makampuni yamefanywa sehemu mbali mbali za dunia, yakitiwa moyo na maandamano ya wiki mbili sasa yanayofanywa New York, ya kupinga biashara ya wafanyakazi wa soko la fedha la mji huo, Wall Street.

Haki miliki ya picha Getty

Maelfu kadha wameandamana katika miji ya Ulaya pamoja na London, Berlin na Athens, baada ya ujumbe kupitishwa kwenye tovuti za kijamii.

Maandamano makubwa kabisa yanatarajiwa mjini Rome na Madrid, ambako wanaharakati, wanaojiita "wenye hasira" wamefanya maandamano kadha mwaka huu.

Hapo awali mamia ya watu waliandamana mjini Hong Kong, Taipei, na Sydney.

Waandamanaji wanalalamika kuwa utajiri mwingi uko mikononi mwa wachache.

Josh Lee ni kati ya waratibu wa maandamano ya Sydney, Australia:

"Hatuzungumzi tu juu ya kubadilisha serikali.

Nafikiri kila mmoja kati yetu hapa anachosema, ni kubadilisha kabisa namna mfumo wetu unavofanya kazi.

Kubadilisha kabisa namna fedha zinavohodhi siasa zetu.

Makampuni makubwa, tunazungumza asili-mia-moja ya watu wa dunia, haya makampuni ya machimbo, mabenki na kadhalika.

Hayo ndiyo yana kauli katika uongozi wa siasa zetu piya.

Vyama vyote viwili vikubwa vya Australia, kwa kweli ni watumishi wa matajiri."