Ocampo awasili Ivory Coast

Ocampo Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ocampo

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ICC, Luis Moreno-Ocampo amewasili nchini Ivory Coast kuchunguza ghasia za bada ya uchaguzi.

Bw Moreno-Ocampo atakutana na waathirika wa ghasia hizo pamoja na wawakilishi wa serikali na vyama vya upinzani waktika ziara hiyo.

Takriban watu 3,000 waliuawa na wengine laki tano kukimbia makazi yao kwa miezi kadhaa wakati wa machafuko ya baada ya upigaji kura mwezi Novemba mwaka 2010.

Majeshi yanayomtii rais Allasane Ouattara na yanayomtii mpinzani wake Laurent Gbagbo yametuhumiwa kwa kutesa watu.

Matokeo

Bw Ouattara aliingia madarakani mapema mwezi Mei kufuatia miezi mitano ya mvutano na Bw Gbagbo ambaye aligoma kukubali matokeo ya uchaguzi.

Bw Moreno-Ocampo amesema "ameishukuru serikali kwa mualiko" uliofanikisha kufankisha ziara yake, mara baada ya kukutana na Waziri Mkuu Guillaume Soro alipowasili.

"Tungependa kuisaidia Ivory Coast kuendelea mbele," amewaambia wandishi wa habari, na kongeza "Tutatenda haki."

Mapemwa mwezi huu, majaji wa ICC walimpa Bw Moreno-Ocampo idhini ya kufanya uchunguzi wa suala hilo.

Uhalifu wa kivita

Wakati uamuzi huo ukitolewa, walisema kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa majeshi yaliyokuwa wakiwatii viongozi wa pande hizo mbili yalifanya uhalifu wa kivita, na uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Uchaguzi wa mwezi Novemba ulidhamiriwa kuiunganisha nchi hiyo, iliyogawanyika kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002.

Ivory Coast - nchi inayozalisha kakao kwa wingi duniani - ilikuwa ikionekana kama kisiwa cha amani katika eneo la magharibi mwa Afrika.

Lakini katika hali halisi, nchi hiyo ilikuwa imegawanyika katika misingi ya kikabila, kidini na kiuchumi.

Bw Gbagbo, ambaye alitawala kwa zaidi ya miaka kumi, yuko katika kifungo cha nyumbani na ameshitakiwa kwa uporaji, wizi wa kutumia silaha na ufujaji mali.

Aligoma kukubali matokeo ya uchaguzi, licha ya Umoja wa Mataifa kumtangaza Bw Ouattara kuwa ni mshindi.