Wanajeshi wa Kenya wameingia Somalia

Wanajeshi wa Kenya wamevuka mpaka na kuingia Somalia kuwasaka wapiganaji wa kiislamu wa Al-Shabaab, ambao wanawalaumu kwa utekaji nyara wa wageni kadha katika ardhi ya Kenya.

Wafanyakazi wawili kutoka Uspania wa Shirika la msaada la kimataifa, walitekwa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab siku ya Alkhamisi, na wanawake wengine wawili walitekwa karibu na Lamu, mwambao wa Kenya, na inaaminiwa wamepelekwa Somalia.

Mwandishi wa BBC alioko kaskazini mashariki mwa Kenya anasema wanajeshi wa Kenya waliingia Somalia Jumapili asubuhi.

Na habari alizopata kutoka Somalia zinaarifu kuwa wanajeshi wa Kenya wakiwa na vifaru wameingia hadi kilomita 90 ndani ya Somalia.

Taarifa alizopata kutoka Liboi, kaskazini mwa Kenya, ni kwamba wanajeshi walionekana wakielekea Somalia.

Hatua hiyo inafuata baada ya Waziri wa Usalama wa Kenya, George Saitoti kusema kuwa Kenya itachukua hatua yoyote kudhibiti mipaka na usalama wake, baada ya wanawake wawili wa shirika la msaada la kimataifa, kutekwa nyara katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab.