Vifo kutokana na malaria vyapungua

Haki miliki ya picha BBC World Service

Idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa malaria vimepungua kwa takriban tu asilimia 20 duniani kote katika muongo mmoja uliopita, shirika la afya duniani limesema.

Ripoti mpya imesema theluthi moja ya nchi 108 ambapo malaria ilikuwa imeenea ulitarajiwa kutokomeza ugonjwa huo katika kipindi cha miaka 10.

Wataalamu walisema kama malengo yataendelea kufikiwa, maisha ya watu wengine milioni tatu yanaweza kuokolewa ifikapo mwaka 2015.

Malaria ni ugonjwa unaoua zaidi duniani, hasa Afrika.

Mwaka 2009, watu 781,000 wamefariki dunia kutokana na malaria.

Ugonjwa huo unaoenezwa na mbu umeenea zaidi kusini mwa jangwa la Sahara, ambapo asilimia 85 ya vifo vimetokea, wengi wao wakiwa watoto chini ya miaka mitano.

Ripoti ya awali ambayo haikuwa sahihi ilitolewa ikisema idadi ya vifo vimeshuka kwa asilimia 40.

Ugonjwa huo umetokomezwa katika nchi tatu tangu mwaka 2007-Morocco, Turkmenistan na Armenia.

Shirika moja la Roll Back Malaria limedhamiria kutokomeza malaria katika nchi nyingine 10 ifikapo mwisho wa mwaka 2015, zikiwemo nchi za eneo la Ulaya.