Majeshi ya Libya 'yamkamata Gaddafi'

Makamanda kutoka baraza la mpito la Libya wamesema wamemkamata aliyekuwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.

Taarifa hizo zimetolewa baada ya majeshi ya baraza hilo la mpito kudai kudhibiti Sirte, mji alipozaliwa Kanali Gaddafi.

Hakuna uthibitisho huru wa kukamtwa kwake.

Kanali Gaddafi alichukua madaraka nchini Libya mwaka 1969.

Alitolewa madarakani katika machafuko yaliyoanza mwezi Februari.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC unataka akamatwe.

"Amekamatwa. Amejeruhiwa miguu yake yote miwili," afisa wa baraza la mpito la taifa (NTC) Abdel Majid ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Amechukuliwa na gari la kubebea wagonjwa."

Shirika la habari la AFP limemnukuu afisa mwengine wa NTC, Mohamed Leith, akisema Kanali Gaddafi amekamatwa mjini Sirte na "amejeruhiwa vibaya" lakini bado anapumua.