ICC yaihoji Malawi kuhusu Rais Bashir

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Omar al-Bashir

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imeitaka Malawi kueleza kwanini ilishindwa kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir katika ziara yake ya hivi karibuni.

ICC imetoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Bw Bashir kwa mashtaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita wakati wa mgogoro huko Darfur.

Malawi ni moja ya nchi zilizotia saini makubaliano ya kuridhia mahakama ya ICC lakini imesema "si kazi yake" kumkamata Bashir.

Bw Bashir amekana mashtaka hayo, akisema yamechochewa na masuala ya kisiasa.

Umoja wa Afrika ulishawishi hati hiyo ya kukamatwa iahirishwe, ikiishutumu ICC kwa kuchunguza tu madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika na kukamatwa kwa rais wa Sudan kutazuia utafutaji wa amani Drafur.

Bw Bashir alilakiwa na gwaride la heshima alipowasili kwenye mji mkuu, Lilongwe, katika mkutano wa masuala ya biashara mwishoni mwa juma.

Umoja wa Ulaya na makundi ya kutetea haki za binadamu yaliisihi Malawi kumkamata Bw Bashir.

Lakini waziri wa habari Patricia Kaliati aliiambia BBC kwamba wasingeweza kumkamata Bw Bashir kwani alikuwa akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (comesa).

Alisema, " Anakuja kikazi na kukamatwa kwa Rais Bashiri hakutuhusu."

Kenya na Chad, ambao wote nao wametia saini mkataba huo wa ICC, wamemruhusu Bw Bashir kutembelea nchi zao.

ICC imeiandikia Malawi kuiomba kufanya "uangalizi" wa ziara ya Bw Bashir kabla ya Novemba 11.

Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika ni miongoni mwa viongozi wengi wa Afrika wanaoishutumu ICC kwa kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika tu na si maeneo mengine.

Bw Bashir alikuwa rais wa kwanza kushtakiwa na ICC, iliyomshutumu kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita Darfur.