Majeshi ya Kenya yasonga mbele Somalia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wa al-Shabaab

Majeshi ya Kenya yakisaidiwa na ndege za kivita yanasonga kusonga mbele ndani ya Somalia kuelekea mji ulio kilometa 120 (maili 75) mpakani na eneo linalodhibitiwa na wapiganaji wa al-Shabaab.

Serikali ya Kenya inataka kuwasukuma wapiganaji hao mbali na mpaka wake kufuatia matukio ya utekaji nyara ambayo Kenya inawalaumu wapiganaji hao kuhusika.

Msemaji wa jeshi la Kenya Meja Emmannuel Chirchir ameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi vyake vinatarajiwa kufika Afmadow Jumanne.

Al-Shabab imeonya kuwa itafanya mashambulio Kenya iwapo haitaondoa vikosi vyake Somalia.

Kundi la al-Shabaab lenye msimamo mkali linadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia na limekanusha kuhusika na utekekaji nyara wowote.

Limekuwa katika vita na serikali ya mpito ya Somalia ambayo inadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hasa mji mkuu Mogadishu.

Serikali hiyo inayoungwa mkono na UN mjini Mogadishu imekataa kukiri kuwa majeshi ya Kenya yako ndani ya Somalia.

Lakini mwandishi wa BBC eneo la Afrika Mashariki Will Ross anasema vyanzo vya habari vinaonyesha kuwa vikosi vya serikali ya mpito ya Somalia vinafanya kazi pamoja na majeshi ya Kenya ili kuyashambulia maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabaab.

Watu walioshuhudia wanasema maafisa wa al-Shabab wamewalazimisha wenye magari kuyasalimisha kwao ili wapiganaji wayatumie kuelekea Afmadow.

Mwandishi wa BBC anasema kusonga mbele kwa vikosi vya Kenya na Somalia kumepunguzwa kasi na matope baada ya mvua kubwa kunyesha.

Afmadow uko kiasi cha kilometa 90 kutoka barabara kuu kaskazini mwa mji wa bandari Kismayo, eneo ambalo ni ngome kuu ya kiuchumi ya al-Shabaab.