Ukame Pembe ya Afrika ‘bado ni janga kubwa’

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wananchi wa Somalia wanakabiliwa na ukame

Miezi mitatu baada ya baa la njaa kutangazwa Somalia, kiwango cha baa hilo katika Pembe ya Afrika bado kiko juu, maafisa wa Uingereza wamesema.

Waziri wa masuala ya Maendeleo ya Kimataifa nchini Uingereza Andrew Mitchel amesema mamia ya watu hasa watoto wanakufa kila siku.

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotajwa na Bw Mitchell, Misaada ya Uingereza inawalisha zaidi ya watu millioni mbili na laki nne katika ukanda huo.

Msimu wa mvua unaokuja unatarajiwa kusababisha magonjwa kwa wakimbizi wengi walio kwenye makambi.

Somalia pekee, Bw Mitchell alisema; zaidi ya watoto 400,000 wako katika hatari ya kufa.

Afya inapewa kipaumbele katika misaada ya Uingereza ambayo imekuja katika Pembe hiyo huku watu milioni 1.3 wakipewa chanjo ya surua, kwa mfano, wakati watu 400,000 wakipewa dozi ya kuzuia malaria na dawa zitapelekwa punde Somalia.

Wakati mvua zinaweza kuleta athari na vifo, zinaweza pia kuwa sehemu ya kutatua janga la njaa pia.

Zaidi ya watu 200,000 wamepewa msaada wa mbegu na Uingereza kupanda wakati hali itakapoimarika.

Changamoto kubwa imekuwa ni kuwafikia wale wenye mahitaji ndani ya Somalia kwenye maeneo yaliyoathiriwa vikali na migogoro wakati njaa ilipotangazwa rasmi mwezi Julai.

Idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini Ethiopia kutokea kusini mashariki mwa Somalia inazidi kuongezeka.