Kifo cha Kanali Gaddafi cha leta utata

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville Haki miliki ya picha other
Image caption Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville

Afisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu inasema uchunguzi kamili unapaswa kufanywa kuhusu jinsi Muammar Gaddafi alivyokufa.

Akizungumza kutoka makao ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, afisa wa kitengo hicho cha haki za binadamu alielezea, picha za simu ya mkononi kuhusu hali ya kifo chake ni zenye kuchafua roho na kuongeza kwamba sheria ya kimataifa inaharamisha kumua mtu bila kumfikisha mahakamani.

Afisi hiyo ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa inasema utawala wa miaka 42 wa Kanali Gaddafi ulikua wa kimabavu na chini ya utawala huo wananchi wa Libya walikabiliwa na mateso mengi. Lakini hata hivyo maafisa hao wameelezea wasiwasi wao kuhusu jinsi Kanali Gaddafi alivyokufa na wanataka ufafanuzi.

"Tunaamini kuna haja ya kufanywa uchunguzi. Maelezo zaidi yanahitajiwa kuhakikisha kama aliuawa katika mapigano au aliuliwa baada ya kukamatwa kwake. Video mbili za simu ya mkononi ambazo zilijitokeza moja ikimuonyesha akiwa hai na nyingine akiwa amekufa zinachafua roho" Matamshi ya msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville

Afisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema kumuua mtu kiholea ni kukiuka sheria ya kimataifa hata kwa watuhumiwa wa uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya binaadamu - kama alivyotuhumiwa Muammar Gaddafi - inapswa wafikishwe mahakamani . Matamshi haya kutoka Umoja wa Mataifa yanabainisha sio tu Umoja huo una mashaka jinsi kanali Gaddafi alivyouawa kikatili, lakini pia kuvunjika moyo kwamba hatakabiliwa tena na mahakama iliyo wazi. Wataalamu wanasema Kumfikisha mahakamani Kanali Gaddafi kungezituliza nyoyo za wananchi wa Libya.