Rais Zuma awafukuza mawaziri waandamizi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Sicelo Shiceka

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewafukuza kazi mawaziri wawili wanaohusishwa na kashfa za rushwa.

Bw Zuma amewafukuza kazi waziri wa serikali za mitaa Sicelo Shiceka-anayeshutumiwa kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa kisheria na waziri wa kazi za umma Gwen Mahlangu-Nkabinde.

Rais huyo pia amemsimaisha mkuu wa polisi Bheki Cele ambaye pamoja na Bi Mahlangu-Nkabinde wamehusishwa na madai ya kuuza majengo kinyume cha sheria.

Wote watatu wamekataa kuhusika na kufanya jambo lolote kinyume cha sheria.

Mchunguzi maalum wa Afrika kusini, aliyeteuliwa kuchunguza malalamiko dhidi ya maafisa wa serikali, alitoa wito kwa Bw Zuma kuwachukulia hatua.

'Bei zilizopanda sana'

Lakini Thuli Madonsela- mchunguzi maalum anayejulikana Afrika Kusini kama mwendesha mashtaka mkuu- aligundua kuwa Bw Shiceka alitumia zaidi ya dola za kimarekani 68,000 za serikali kwa safari za kifahari na malipo ya hoteli bila idhini.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mkuu wa polisi Bheki Cel

Gharama hizo ni pamoja na safari za kumtembelea mpenzi wake aliyekuwa amefungwa Switzerland kwa makosa ya kufanya magendo ya dawa za kulevya.

Katika ripoti iliyotolewa mwezi uliopita, Bi Madonsela alisema vitendo vya Bw Shiceka vilikuwa "kinyume cha sheria na matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uaminifu kwa fedha za umma."

Alimshutumu pia kwa kusafiri nchi ya jirani ya Lesotho wakati akiwa likizo kutokana na kuumwa kwa gharama za walipa kodi' akitumia jina la uongo.

Kwa wakati huo, Bw Shiceka alikana madai hayo akisema "hayana msingi" na kuahidi kusafisha jina lake mahakamani.

Alielezea baadhi ya gharama zake za hoteli ni kutokana na nyumba aliyopewa kutokana na wadhifa wake kujaa mbu.

Katika uchunguzi tofauti, Bi Madonsela aliamua kwamba Bi Mahlangu-Nkabinde na Jenerali Cele- mshirika mkuu wa Bw Zuma- waliidhinisha mpango wa majengo yenye thamani ya mamilioni ya dola za kimarekani.

Bw Zuma alisema Jenerali Cele atasimamishwa kazi huku akilipwa mshahara wote, na uchunguzi ukiendelea dhidi yake.

Rais huyo alisema, uchunguzi huo utaongozwa na Jaji wa mahakama ya katiba Yvonne Mokgoro.