Rais wa Somalia atofautiana na Kenya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Shambulio limetokea mjini Nairobi

Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, amesema hajaridhia kwa jeshi la Kenya kuingia nchini Somalia.

Katika wiki moja tu iliyopita askari wa Kenya walivuka mpaka kuingia Somalia kupambana na wanamgambo wa kundi la al-Shabab.

Nairobi ilisema kuingia kwao humo kumefanyika kwa ridhaa ya serikali ya Somalia.

Mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki amesema kauli hii ya hivi karibuni itaiweka serikali ya Kenya katika nafasi ngumu.

Alisema Rais Ahmed huenda ameyasema hayo kwasababu anapinga wazo la Kenya la kuanzisha eneo litakalojitawala kusini mwa Somalia.

Watu 13 washambuliwa mjini Nairobi

Shambulio la guruneti katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, limesababisha watu 13 kujeruhiwa, mtu mmoja kati yao alijeruhiwa vibaya.

Guruneti hilo lilirushwa na mtu asiyejulikana. Mtu huyo alifika kwenye eneo hilo la burudani na mlango ulipofunguliwa alirusha guruneti na kukimbia.

'' Mwanamme mmoja aligonga mlango akijifanya kama mteja na aliporuhusiwa kuingia ndani, akarusha guruneti'' alisema mkuu wa polisi mjini Nairobi, Anthony Kibuchi.

Wengi walijeruhiwa katika sehemu za mikono na miguu.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu. Majeruhi walikimbizwa katika hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta.

Shambulio hili linatokea wiki moja baada ya vikosi vya Kenya kuingia nchini Somalia kukabiliana na wapiganaji wa al-Shabaab, ambao Kenya inawashtumu kwa mashambulio na utekaji nyara wa watalii.

Al-Shabaab walitishia kufanya mashambulio kutokana na hatua hiyo ya Kenya.