Chinamasa amshambulia Tsvangirai

Trvangirai Haki miliki ya picha AFP
Image caption Morgan Tsvangirai amezua mjadala kuhusu msimamo wake juu ya haki za wapenzi wa jinsia moja

Waziri wa sheria wa Zimbabwe Patrick Chinamasa ametupilia mbali wito wa Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai kujumuisha haki za wapenzi wa jinsia moja katika katiba mpya.

Bw Chinamasa ameiambia BBC kuwa haki za wapenzi wa jinsia moja haziwezi kuingizwa "kinyemela" ndani ya katiba kwa sababu Wazimbabwe wengi wanapinga jambo hilo.

Mapema, Bw Tsvangirai aliiambia BBC kuwa haki za wapenzi wa jinsia moja ni "haki za kibinadamu" na lazima ziheshimiwe.

Bw Tsvangirai na Bw Chinamasa wanatoka vyama hasimu lakini wapo pamoja katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Vyama vyao - MDC na Zanu-PF vinaandaa muswada wa katiba mpya ambayo itapigiwa kura ya maoni kabla ya uchaguzi mwaka ujao.

Mapenzi ya jinsia moja ni marufuku kwa sasa nchini Zimbabwe, kama ilivyo katika nchi nyingi za kiafrika ambapo watu huona sheria za wapenzi wa jinsia moja ni kinyume na Ukristo na sio Uafrika.

Mwaka jana, Bw Tsvangirai alisema "mababu zetu watatikisika ndani ya makaburi yao" iwapo haki za wapenzi wa jinsia moja zitawekwa katika katiba mpya. Lakini Bw Tsvangirai alionekana kubadili msimamo wake katika mahojiano na kipindi cha Newsnight cha BBC.

"Ni jambo lenye utata katika eneo nitokalo. Mtazamo wangu ni kuwa natumaini katiba mpya itakuwa na uhuru wa kuamua suala la jinsia, ikiwa tu haimuingilii mtu yeyote," alisema Bw Tsvangirai.

"kwangu mimi, hii ni haki ya kibinadamu."

Huwezi kusikiliza tena

Kujibu hoja hiyo hilo, Bw Chinamasa alisema Wazimbabwe walikataa haki za wapenzi wa jinsia moja wakati walipoulizwa kwenye mradi wa serikali kuhusu katiba mpya.

"Wote tunafahamu watu walichosema kuhusu wapenzi wa jinsia moja -- ni hapana; kwa karibu asilimia 100 hapana," alisema Bw Chinamasa akizungumza na kipindi cha Network Africa cha BBC.

Bw Chinamasa alisema Bw Tsvangirai alitoa matamshi hayo kwa ajili ya lengo la propaganda, akiwa tofauti na msimamo wake wakati alipoingia madarakani. "Hatuwezi kuingiza kimagendo ndani ya katiba maoni ya waziri mkuu ambaye anataka kuridhisha watu fulani, au labda kujitafutia uwezo ndani ya chama chake."

"Nafahamu kibinafsi haamini jambo hilo. Amesema mara nyingi ndani ya baraza la mawaziri," Bw Chinamasa ameiambia BBC.

Uchaguzi unaotazamiwa mwakani utakuwa wa kwanza tangu vyama vya MDC na Zanu-PF vinavyoongozwa na Rais Robert Mugabe - kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa mwaka 2008.

Uchaguzi huo ulizongwa na ghasia na wizi wa kura, na Bw Tsvangirai kususia uchaguzi wa duru ya pili.

Serikali ya umoja wa kitaifa - iliyoundwa kutokana na shinikizo kutoka kwa viongozi wa eneo hilo - ilileta utulivu nchini humo, lakini mvutano umekuwa ukiongezeka kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao.

Vyama hivyo viwili bado havijakubaliana kuhusu mabadiliko ya kiusalama na kisiasa ili kuhakikisha uchaguzi ulio huru na wenye haki.