Tuzo kwa wanaharakati

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mohamed Bouazizi

Wanaharakati watano waliochochea mabadiliko kwenye nchi za Kiarabu wameshinda tuzo ya bunge la Ulaya la Sakharov inayohusu uhuru wa fikra.

Washindi hao ni Mohamed Bouazizi wa Tunisia, ambaye kifo chake mwezi Januari kilisaidia kuchochea vuguvugu la mabadiliko katika nchi za kiarabu.

Alijiwasha moto Desemba iliyopita kupinga mambo aliyofanyiwa na mamalaka ya nchi hiyo chini ya uongozi wa rais aliyeondolewa Zine el-Abidine Ben Ali.

Tuzo hiyo, iliyopewa jina la daktari wa Kisovieti na mpinzani Andrei Sakharov, ina zawadi ya euro 50,000.

Washindi wengine wa tuzo hiyo ni Asmaa Mahfouz, muasisi wa vuguvugu la vijana la Aprili 6, mpinzani wa Libya Ahmed al-Zubair Ahmed al-Sanusi; na Wasyria wawili ambao ni sehemu ya vuguvugu kwa sasa nchini mwao, wakili Razan Zeitouneh na mchora vibonzo Ali Farzat.

Bi Mahfouz ambaye alitoa wito wa kutaka uhuru kupitia mtandao, iliyosomwa na maelfu ya watu, ilisaidia kuwapa moyo waandamanaji wa eneo la wazi la Tahrir iliyosababisha kujiuzulu kwa Rais wa Misri Hosni Mubarak.

Alikamatwa kwa mashtaka ya kukashifu wakuu wa kijeshi waliochukua madaraka kufuatia kuondoka Bw Mubarak, lakini mashtaka hayo yalifutwa baadae kutokana na maandamano.

Bw Sanusi alikaa jela miaka 31 kwa kumpinga Kanali Muammar Gaddafi.

Bw Zeitouneh ni mmoja wa viongozi wa kamati zilizoshiriki kwenye machafuko dhidi ya Rais Bashar al-Assad.

Bi Farzat ni mchora vibonzo maarufu Syria ambaye alipigwa na majeshi ya usalama mwezi Agosti, na kusababisha kuvunjwa kwa mikono yake yote miwili.

Tuzo ya Sakharov imekuwa ikitolewa na bunge la Ulaya tangu mwaka 1988 kwa watu binafsi na mashirika yaliyotoa mchango muhimu kwa mapambano ya haki za binadamu na demokrasia.

Washindi waliopita ni pamoja na rais wa kwanza Mwafrika, Nelson Mandela, na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.