Tunisia - Matokeo yazusha rabsha

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Matokeo ya uchaguzi wa Jumapili yamezua rabsha

Makabiliano makali yamezuka kati ya polisi na waandamanaji nchini Tunisia katika mji wa kati ya nchi wa Sidi Bouzid ambao ni chimbuko la mapinduzi ya raia yaliyomng'oa mamlakani aliyekuwa rais Zine el-Abidine Ben Ali mwezi Januari.

Polisi wamelazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wakilalamikia uamuzi wa tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya maeneo kadhaa.

Tume ilifuta matokeo katika maeneo yaliyokuwa yameshindwa na chama kimoja cha kisiasa kilichoshiriki uchaguzi wa bunge jipya Jumapili iliyopita.

Chama hicho kinadaiwa kukiuka sheria za uchaguzi.

Waandamanaji hao walivamia ofisi za tawi la chama kilichoshinda uchaguzi huu cha kiislamu chenye msimamo wa wastani,Ennahda.

Awali tume hiyo ilikuwa imethibitisha rasmi kuwa chama hicho cha Ennahda,kilishinda uchaguzi huu.