Saif Gaddafi asema hana hatia

Mkuu wa mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa, ICC, anasema mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi, Saif al Islam, anajitetea kuwa hana makosa.

Haki miliki ya picha Reuters

Saif Gaddafi amejificha, baada ya serikali ya baba yake kutolewa madarakani.

Luis Moreno-Ocampo anasema Saif, kwa kupitia wajumbe, amemwambia kuwa anataka kufutiwa mashtaka.

Luis Moreno-Ocampo anasema Saif Gaddafi amekuwa na hamu ya kutaka kujua hatima yake, endapo ICC itamkuta hana makosa.

Yeye anakanusha kuwa aliamrisha mashambulio ya mabomu na risasi dhidi ya waandamanaji mwezi wa Februari, wakati maandamano yalipoanza nchini Libya; na anasema anaweza kutoa ushahidi kuonesha kuwa hana hatia.

Mahakama ya ICC yamemshtaki Saif Gaddafi, hayati baba yake, Kanali Gaddafi, na mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi Abdullah al-Senussi, na uhalifu wa kivita.

Bwana Moreno-Ocampo anataka kumfikisha The Hague mtoto wa Kanali Gaddafi, ili kuanza kesi.

Anajua kuwa Saif anajaribu kuchunguza yanayomkabili, pamoja na kuzungumza na nchi chache ambazo zinaweza kumpa hifadhi na askari mamluki wanaoweza kumpeleka huko.