Kesi ya Mubarak yaahirishwa tena

Kesi ya rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, imeakhirishwa hadi mwisho wa Disemba.

Haki miliki ya picha AFP

Hayo yalitangazwa wakati majadiliano yanaendelea kama jaji anafaa kubadilishwa.

Hosni Mubarak, jamaa zake, na wakuu wa usalama, wanashutumiwa kuwa waliamrisha mauaji ya waandamanaji mapema mwaka huu.

Katika kikao kifupi cha mahakama mjini Cairo Jumapili, Jaji Ahmed Refaat aliakhirisha kesi ya Hosni Mubarak na wenzake walioshtakiwa pamoja, hadi mwisho wa mwezi Disemba.

Jopo linazingatia ikiwa majaji wanaoendesha kesi wabadilishwe, baada ya malalamiko ya mawakili wa familia za watu waliouwawa katika maandamano awali mwaka huu.

Kesi hiyo imekuwa ikiendelea na kusita, tangu mwezi Agosti.

Lakini hakuna hakika kuwa hata ikifika Disemba kesi hiyo itaendelea, kwa sababu imeripotiwa kuwa hata wajumbe wa jopo linalofikiria kama majaji wabadilishwe, wao wenyewe piya wamejiuzulu.

Hatua hiyo itawakera Wamisri wengi, ambao siku zote wamekuwa wakishuku kuwa viongozi wepya wa kijeshi wanachelewesha mambo, kwa sababu hawataki kukabili matatizo yatayozuka endapo Hosni Mubarak atakutikana na hatia au la.